USALAMA JUKUMU LETU
1. BIISMILLAHI AHADI
KWA INA LAKE WADUDI
ALIFARIDU SWAMADI
INA LAKE NAANDIYA
2. NIMSWALIYE HABIBU
NIUTIMIZE WAJIBU
NDO NIANDE KUKUTUBU
NUDHUMU KUITUNGIYA
3. MADA HII KUBWA SANA
NI NDEFU PIA NI PANA
ANIAFIQI RABBANA
YOTE KUIMALIZIYA.
4. SALAMA NI KUTOKUWA
NA WASI WASI KUNGIWA
UKETIPO KUPUMUWA
MAKINI UMETULIYA.
5. USALAMA MBWA NAFUSI
USALAMA MBWA UNASI
ALIYE JINI NA NSI
USALAMA HULILIYA.
6. USALAMA MBWA MUILI
MARADHI KUTOQABILI
USALAMA NI WA MALI
WIZI KUTOKUVAMIYA.
7. USALAMA WA AKILI
ILIMU SIO JUHALI
NA ULEVI SAMPULI
KUTOPATA KUINGIYA.
8. NA USALAMA WA HALI
KILA ZAMA NA MAHALI
MTU IWE NI MUHALI
MADHARA KUMTOKEYA.
9. HAPO ZAMANI ZA KALE
AMU YETU AMU ILE
USALAMA ULITELE
WAZEE WANATWAMBIYA
10. WATU WALIKIYUWANA
NA WAKIKIRIMIANA
HAKI WAKITUNDIANA
USALAMA UKENEYA.
11. UTEMBEAPO NDIANI
UKETIPO BARAZANI
UBUKHERI WA AMANI
HAKUNA LAKUTOKEYA.
12. USALAMA ULOKUWA
MPAKA TWAHADITHIWA
AMU WALIYAMKUWA
MAKA TOTO TWASIKIYA.
13. YEO SALAMA HAKUNA
NYUMBA HUVUNDWA NTANA
WALEVI WAMEYAZANA
MAJAMBAZI WAMEYAA.
14. WANENDAPO HARUSINI
WAKE HUSITA ZIDANI
NA ZIPULI NA HERINI
KUNYANG’ANYWA WAHOFIYA.
15. SUALI NAJIULIZA
HUWAZUA NA KUWAZA
NI NANI ALIYEANZA
MAMBO HAYA KUTWETEYA.
16. TANENA HAPA SISITI
TWAWAYUWA WAVUNDATI
SIKU ZOTE NI WANATI
NA WAGENI WAKANGIYA.
17. TUMUATAPO MMOYA
WAWILI WATATU PIYA
NYUNGA WAKITUZANYIYA
NI NNI TWATARAJIYA?
18. BAROBARO WATANGIYA
KWENYE NYUNGA KUTUMIYA
WAKISINDIA NA NDIYA
NANI MUI TANGALIYA?
19. TUKIKIRI TEMBO KUYA
BOTI NZIMA KUNGIYA
MADUKA KUZANYA PIYA
MWISHOWE TWAFIKIRIYA?
20. WALEVI KUTUSUMBUWA
BANATI TUKISHIKIWA
ZIKUMBO TUKIPIJIWA
JEE TWAYATAKA HAYA?
21. TUWAATAPO WAGENI
WASO KAZI WALA DINI
WALALE VIBARAZANI
MUINI MWETU KUYAA
22. TAKUWA TWAFUGA WIZI
WALAGHAI MAJAMBAZI
WASO KAZI WALA BAZI
KAZI NI KUTUVAMIYA.
23. TUSIPOPEKA ZUONI
WANA KUIYUWA DINI
KUTOWAPEKA SHULENI
VIZAZI GANI TWALEYA?
24. TWALEYA WATU WAZIVU
WASOZITUMIYA NGUVU
WANGOJEA ZILO MBIVU
NAZI KUWAANGUKIYA.
25. WATAKA WAO WAPEWE
WATAKACHO WAETEWE
WASIPOPATA WENYEWE
UHUNI KUINGILIYA.
26. TUSILIE NA POLISI
POLISI NI SISI SISI
KULINDA ZETU NAFUSI
NA UMATI WOTE PIYA.
27. NI LETU SOTE JUKUMU
KUILINDA YETU AMU
MALINDI HATA WATAMU
NA NCHI YOTE PAMOYA.
28. SOTE TUHIMIZANENI
KUPEKA WANA SHULENI
TUSIKUBALI WAGENI
WASIO PA KWELEKEYA.
29. TUSIKUBALI WALEVI
WALA WAUZA WALEVI
AMA TUTAFUGA WIVI
LA BUDA NIMEWAMBIYA.
30. WALE WATU WAUZAO
TEMBO BANGI NYUNGA ZAO
NI ADUI WATU HAO
TUWATOWE MUI PIYA.
31. TUJITAHIDI TUFANYE
TUPATILIZE PENYENYE
KILIO HULIA MWENYE
NA MTU MBALI KALIYA.
32. RABBI TUPE USALAMA
UTWENEE SOTE UMMA
DUNIANI NA QUYAMA
WASALAMA NAKOMEYA.
--TAMAT--
©BHADDY SHEE 14 DHULHIJJAH 1432/ 9.NOV.2011
No comments:
Post a Comment